
Uchunguzi
mpya umeonyesha kwamba watu wanaweza kukabiliana kirahisi na magonjwa
mbalimbali kwa kula matunda ya aina mbalimbali na mboga mboga badala ya
kuongeza idadi ya matunda na mboga mboga hizo. Kwa mujibu wa uchunguzi
huo uliotolewa katika Kongamano la Majaribio ya Kibiolojia huko Anahein
California, baadhi ya matunda na mboga mboga yana faida kubwa ya lishe
kuliko mengineyo. Uchunguzi huo umeeleza kwamba,ingawa karoti inaaminiwa
kuwa ni chanzo kikubwa cha beta-carotene lakini kula viazi vitamu
badala ya karoti kunaweza kuupatia mwili beta-carotene mara dufu kuliko
karoti. Papai nalo lina beta-cryptoxanthin mara 15 zaidi ya machungwa.
Halikadhalika mboga aina ya Kale huupatia mwili mada ya
lutein/zeaxanthin mara tatu zaidi ya spinachi. Pia imeelezwa kuwa
stroberi na rasberi zina ellagic asid mara tatu zaidi huku kikombe
kimoja cha maji yanayotokana na mmea uotao majini wa watercress ikiwa na
mada ya isothiocyanate sawa na inayopatikana katika vijiko vine vya
chai vya haradali au mustard. Bi. Keith Rabdolph aliyeongeza uchunguzi
huo anashauri kwamba, watu wajitahidi kujua umuhimu wa vyakula
wanavyokula na kujua pia ubora na faida za matunda na mboga mboga
wanazokula kwa afya ya miili yao.

Imetahadharishwa
kwamba kulala usingizi wa chini ya masaa 6 kila usiku kunaweza
kusababisha mtu apatwe na kifo cha mapema. Watafiti wamesema kuwa watu
ambao kwa kawaida huwa wanalala masaa hayo machache wengi wao hupatwa na
vifo vya mapema kwa asilimia 12 zaidi ya wale wanaolala kawaida kwa
masaa 8. Vifo ambavyo hutokea katika umri wa baada ya miaka 25. Pia
imeonyeshwa kwamba kulala zaidi ya masaa 9 pia kunapelekea vifo vya
mapema ingawa kulala huko kunaweza kukawa na uhusiano na matatizo ya
kiafya. Utafiti huo umetolewa kwa kuchunguzwa uhusiano uliopo kati ya
kifo na usingizi kwa kutegemea chunguzi 16 zilizofanywa kwa
kuwahusisha watu milioni 1 na nusu katika nchi za Uingereza, Marekani ,
Ulaya na Mashariki mwa Asia.
Profesa Francesco Cappiccio aliyeongeza
utafiti huo wa chuo kikuu cha Warwick cha Uingereza anasema jamii za
hivi sasa zilizoendelea zimekuwa taratibu zikipunguza muda wa kulala,
na tatizo hili linawapata sana watu wanaofanya kazi masaa mengi. Amesema
suala hili linaonyesha kwamba hayo yote yanatokana na mashinikizo ya
kimaisha yanayowapelekea watu wafanye kazi masaa mengi na kuchukua shift
nyingi za kazi. Amesema kwamba, kuporomoka kwa afya kunaambatana na
kulala masaa mengi zaidi. Wataalamu wanasema kuwa, watu wanapaswa
kufahamu kwa nini hasa usingizi ni suala muhimu sana kwa afya nzuri.
Usingizi ni kama karatasi ya litmus inayoonyesha afya na hali ya mwili
na akili ya mtu kwani usingizi unaathiriwa na magonjwa na hali
mbalimbali ikiwemo msongamano wa mawazo au depression, anasema mtaalamu
huyo. Inashauriwa kuwa tusilale masaa machache wala mengi bali tulala
kwa masaa ya wastani ambayo ni masaa 8.

Mwanamke
wa Kijapan aliyevunja rikodi ya Dunia ya Guinness kwa kuwa mtu mzee
zaidi duniani amefariki dunia siku kadhaa zilizopita, akiwa na umri wa
miaka 114 na siku 357. Mwanamke huyo aitwaye Kama Chinen alikuwa
akiishi katika kisiwa cha Okinawa na alifariki dunia Mei 2, ambapo
aliishi na kushuhudia karne tatu!. Inasemekana kuwa bibi huyo aliishi
muda mrefu kwa kuwa lishe yake ilikuwa chai ya kijani, supu ya miso,
mboga mboga, wali na samaki freshi. Bi. Chinen sio makazi pekee wa eneo
hilo la Japan aliyeishi muda mrefu, kwani ripoti zinasema kuwa watu
wengi wanaoishi eneo hilo huishi maisha marefu na ni kutokana na lishe
yao. Japan ndio nchi inayoongoza kwa kuwa na kiwango kirefu zaidi cha
maisha ya watu (Highest Life Expactancy) huku Okinawa ukiwa mji ulio na
watu wengi wenye umri mrefu, suala ambalo linatokana na lishe bora na
hali ya hewa ya kisiwa hicho.
Kwa mujibu wa utafiti, mji wa Okinawa
una kiasi kidogo sana cha watu wenye magonjwa ya kensa, na hiyo
inatokana na watu kula vyakula vyenye mafuta kidogo, kalori chache,
ufumwele kwa wingi na mboga mboga na matunda kwa kiasi kikubwa. Pia
suala lingine ni kujishughulisha kwao na wala sio kukaa tu

Wadau
msichoke na mimi kuzungumzia ugonjwa wa moyo, au nisiseme mimi, bali
niseme wataalamu ambao kila siku wamekuwa wakifanya majaribio na
kutuelewesha vyakula au njia zinazotuepusha na ugonjwa huu. Hii ni kwa
sababu ugonjwa wa moyo kweli ni tishio duniani kote. Ni wiki iliyopita
tu mfanyakazi mwenzangu ambaye nilikuwa naye kazini hadi nyakati za
mwisho za kazi, siku ya pili nakuja kazini naambiwa kafariki dunia kwa
mshituko wa moyo. Masikini baba wa watu!!, huku akiwa anayetegemewa na
familia, akiacha mke na mtoto ameondoka kama utani tena kwa kufumba na
kufumbua. Baada ya kutoka kazini alikaa juu ya kochi na kujiegemeza
akisubiri atengewe msosi, lakini hapo hapo aliaga dunia. Msosi
ulipotengwa na mkewe kumuamsha ale akidhani labda amepitiwa na usingizi,
aliona haamki tena, na ndipo walipomkimbiza hospitalini. Huko
waliambiwa ameshakufa zamaaani kutokana na mshituko wa moyo!.
Sasa
hali ni hii, na hivi karibuni uchunguzi mpya umeonyesha kwamba kula
zabibu au vyakula vyenye zabibu ndani yake kunapunguza shinikizo la
damu, husaidia moyo kufanya kazi zake vyema na kupunguza hatari ya
kupatwa na ugonjwa wa moyo.
Kwa mujibu wa uchunguzi huo uliotolewa
kenye mkutano wa Majaribio ya Bayolojia huko California, zabibi zina
uwezo wa kupunguza shinikio la damu, husaidia mwili uweze kuvumilia
sukari (glucose tolorance) na kupunguza kiwango cha mafuta aina ya
triglycerides mwilini ambayo ni chanzo cha matatizo ya moyo.

Wataalamu
wanasema zabibu pia zinaweza kupunguza uvimbe, uharibivu unaotokana na
free radicals zinazozalishwa mwilini na shinikizo la moyo.
Kwa
ujumla zabibi zinazuia hali inayoitwa Metabolic Syndrome suala ambalo
linatokana na mada za phytochemicals zilizoko kwenye matunda hayo.
Metabolic
Syndrome ni mchanganyiko wa matatizo ya kitiba ambayo yanaongeza
uwezekano wa kupatwa na maradhi ya mishipa ya damu pamoja na kisukari.
Hivyo
wataalamu wanatushauri tule zabibi au kuongeza zabibu katika vyakula
wanavyokula kila siku, ili tujikinge na ugonjwa wa Metabolic Syndrome,
ugonjwa wa moyo na kisukari aina ya pili.
Haya shime tule zabibu kwa ajili ya afya zetu!.
Wapenzi wadau natumaini hamjambo! kumekuwa na baadhi ya wadau
wanaoniandikia na kuomba ushauri mbalimbali kutokana na matatizo
waliyonayo. Nawashukuru sana kwa kuwa wanafuatilia yale yanayojiri
katika blogi hii na kupata ingawa machache kuhusiana na afya zetu. Pia
nawashukuru kwa kuniwezesha nami kuzungumzia mada mbalimbali kutokana
na maswali yenu munayoyauliza. Kwa wale wenye maswali na matatizo
mbalimbali tafadhali sana niandikieni kwa kupitia email yangu ambayo ni
sthugs4j@gmail.com. Kwani wale wanaoandika maswali yao katika sehemu ya
maoni, baadhi ya wakati huwa siyaoni katika muda unaotakiwa na hivyo
hunifanya nichelewe kuwajibu. Wote mnashukuriwa. Leo tutazungumzia suala
la kujihisi uchovu wakati wa ujauzito ambalo limeulizwa na mmoja wa
wadau wanaofuatilia kwa karibu kona ya afya nami nalijibu swali lake
kama ifuatavyo.

Wanawake
wengi kwa kawaida huwa wanahisi uchovu wakati wa ujauzito. Uchovu,
kulegea mwili na kuishiwa na nguvu ni jambo la kawaida katika kipindi
hicho. Hii ni kwa sababu mwili katika kipindi hiki unatumia nguvu za
kiada ili kuunda kiumbe kipya. Pia wakati huu mwili hutengeneza damu kwa
wingi zaidi ili kufikisha chembechembe za chakula kwa mtoto, suala
ambalo huufanya mwili ufanye kazi ya ziada na hata viungo vingine muhimu
kama vile moyo na vinginevyo. Uzito wa mtoto nao unaoongezeka katika
mwili wa mama mjamzito siku baada ya siku, ni sababu nyingine
inayomfanya mama mjamzito ajihisi kuchoka. Kuchoka au kiushiwa na nguvu
ni tatizo la kawaida hasa katika miezi mitatu ya mwanzo ya mimba.
Katika miezi hiyo ya mwanzo ya mimba tatizo hilo husababishwa na
mabadiliko ya homoni za mimba mwilini hasa progestrogen na wakati
mwingine hali hiyo huongezwa na kichefuchefu na kutapika. Hali hiyo ya
mchoko inatarajiwa kuisha inapoingia miezi mitatu ya pili ya mimba.
Lakini pia kuna wengine ambao hali hiyo ya kuchoka huendelea nayo hadi
wakati wa kujifungua. Kushindwa kulala vizuri kutokana na kwenda mara
kwa mara msalani, au kukosa uzingizi kutokana na ongezeko la ukubwa wa
tumbo mwishoni mwa ujauzito, ni miongoni mwa masuala ambayo humfanya
mama mjazito ajisikie mchovu na akose nguvu siku nzima.
Vilevile
mabadiliko ya kifizikia na kisaikolojia ya wakati wa ujauzito humfanya
mama mjamzito awe na morali ya chini na kuhisi uchovu wa kimwili na
hata kiakili. Sababu nyinginezo zinaweza kutokana na kazi mbalimbali
anazofanya mama huyo au pia ukosefu wa lishe inayofaa na ya kutosha kwa
ajili ya mwili wake, ambao unahitajia nguvu ya ziada hasa kwa ajili ya
uumbaji wa ukamilifu wa mtoto aliye tumboni.
La muhimu analoshauriwa
mama mjamzito ni kutoogopa na kutotishwa na hali hiyo, kwani inatokana
na baadhi ya mabadiliko yanayotokea katika mwili wake. La muhimu ni mama
mjamzito kufuata ushauri unaotakiwa ili kukabilina na hali hiyo.
Zifuatazo ni njia za kukabiliana na uchovu wakati wa ujauzito.
•
Kwanza kabisa mama mjamzito anatakiwa ale vyema. Mama mjamzito
anatakiwa ale chakula bora na kamili, chenye kalori 300 au 500 za ziada
ikilinganishwa na mtu asiye mjamzito kwa siku. Lakini awe mwangalifu na
ni bora akigawe chakula chake katika sehemu ndogo ndogo 5 au 6 (suala
hili tumelizunguzia kwa undani katika makala iliyopita ya kiungulia
wakati wa ujauzito, tafadhali pitia makala hizo). Anaweza akawa akibeba
matunda na mboga mboga kama asusa (snacks) kwa ajili ya kula kila
anapohisi njaa popote pale awapo. Lakini ni bora ajiepushe na vyakula
vyenye sukari nyingi na caffeine, kwani vyakula hivyo huyeyuka haraka
mwilini na kumfanya ahisi njaa mapema.
• Mama mjamzito ahakikishe
kuwa hana upungufu wa damu. Na kama anao basi atumie dawa za kuongeza
damu zinazotolewa na madaktari, au ale vyakula vinavyoongeza damu. Hii
ni kwa sababu ukosefu wa madini ya chuma mwilini unaosababisha ukosefu
wa damu, ni miongoni mwa sababu zinazomfanya mama mjamzito ahisi
kuchoka. Mtu mwenye ukosefu wa damu (Anemia) huhisi kubanwa na pumzi,
ongezeko la mapigo ya moyo, udhaifu, kupauka na kizunguzungu. Onana na
daktari iwapo una dalili kama hizo.

•
Mama wajawazito wanashauri kujipumzisha nyakati za mchana. Ni bora mama
mjamzito apumzike kwa kadri anavyoweza wakati wa mchana, baada ya
chakula cha mchana au hata kabla ya nyakati za magharibi. Ikiwa unafanya
kazi, basi pumzika mara kwa mara japo kwa muda mfupi ili kufanya mwili
upate nguvu.
• Mama wajawazito wanashauriwa kujitahidi kulala mapema,
hasa kama ikiwa inakubidi uamke mara kadhaa usiku kutokana na sababu
mbalimbali, kama vile kwenda msalani, kula au kutokana na maumivu.
•
Kufanya mzoeni husaidia kupunguza uchovu na kuna faida kemkem wakati wa
ujauzito. Kahusiana na suala hilo soma makala zilizotangulia.
• Mama mjamzito anatakiwa anywe maji ya kutosha. Ukosefu wa maji mwilini huchangia kumfanya mama mjamzito ahisi uchovu.
•
Usifanye kazi nyingi kutwa nzima, na kama inawezekana ni bora usaidiwe
kazi hizo hasa za nyumbani na watu wengine katika familia kama vile
watoto, mume ndugu, jamaa na marafiki.
• Usikilize mwili wako. Pale unaposikia njaa basi kula na pale unapojisikia uchovu jitahidi upumzike.
•
Pata ushauri wa daktari iwapo unahisi uchovu wa kupindukia au unachoka
kila mara, ili uwe na uhakika kuwa hakuna tatizo au hatari inayoweza
kuhatarisha maisha yako na ya mtoto.

Watafiti
wa Canada wamesema kuwa, kuwapa watoto sukari kabla ya kupewa chanjo
kunapunguza maumivu. Watafiti wa Chuo Kikuu cha Toronto wamesema kwamba
watoto wachanga wakipewa matone machache ya maji ya sukari, kabla ya
chanjo hawatolia au watapunguza kulia. Hayo yamesemwa baada ya watoto
1,000 wachanga kupewa maji ya glukosi kabla ya kupigwa sindano na
kupunguza kulia kwa asilimia 20. Utafiti huo umechapishwa katika jarida
la Mafanikio ya Magonjwa ya watoto na umetokana na matokeo ya majaribio
14 yaliyofanywa kuhusiana na suala hilo. DaktaArme Ohlsson aliyeongoza
timu ya utafiti huo amesema kwamba umefanywa kwa watoto wasiozidi mwaka
mmoja. Pia watatifi hao wamesema kwamba, matone machache tu au nusu
kijiko cha maji ya glukosi au sackrosi pia hupunguza muda wa mtoto
kulia. Pia wamewashauri maafisa wa afya wawape watoto sakrosi na
glukosi kabla ya kuwapatia chanjo. Wamesema kwa kuwa vyakula vitamu
vina uwezo wa kupunguza maumivu ndio sababu watoto wanapopewa glukosi
kabla ya chanzo huwa hawalii.

Taarifa
mpya zinasema kwamba, maafisa wa afya wametahadharisha juu ya kutumiwa
kwa muda mrefu dozi kubwa ya dawa za kuondoa kiungulia, (heartburn) na
kusisitiza kwamba zinasababisha mifupa kupasuka. Dawa hizo ni zile
zinazojulakana kama Proton Pumping Inhibitors (PPI) zinazozuia kiungulia
na ambazo hutumiwa kudhibiti kiwango cha asidi katika tumbo na pia
kutibu ugonjwa wa GERD au gastroesophageal reflux disease. Taarifa hizo
zilizotolewa na Kitengo cha Kusimamia Vyakula na Dawa cha Marekani (FDA)
zinasema kwamba, dawa hizo za kingulia huongeza uwezekano wa kupasuka
mifupa ya nyonga (hip), mikono na ute wa mgongo kwa watu wazima, hasa
iwapo dawa hizo zitatumiwa kwa mwaka mmoja au zaidi, au kwa dozi kubwa.
Joyce
Korvick Mkurugenzi wa masuala ya usalama wa kitengo cha FDA anasema
kwamba, kwa kuwa dawa hizo zinatumiwa sana na watu wengi, ni muhimu kwa
watu wote kufahamu madhara yanayoweza kusababishwa na dawa hizo. Maafisa
hao pia wamewataka madaktari kuwaandikia tu dawa hizo wagonjwa ambao
hali zao ni mbaya mno, na kusisitiza kuwa faida ya dawa hizo pale
zinapotumiwa mara chache ni zaidi ya hatari inayozisababisha.
Huko
nyuma pia wataalamu walisema kwamba, dawa hizo za kutibu kiungulia
zinahusiana na ongezeko la hatari ya maambukizo ya bacteria aina ya C.
difficile anayesababisha ugonjwa wa kuharisha.
Dawa hizo ni kama
zile za Emsomeprazole, Dexlansoprazole, Lansoprazole, Emprazole/Sodium
Bicarbonate, Pantoprazole, Rabeprazole na Rabeprazole.
Ndugu mdau kama wewe ni miongoni mwa wanaotumia dawa hizo, basi jihadhari kabla ya hatari!