Mungu akisema ndiyo
Ujapo uamkio, kujihimu kwa mapema,
Ushike kitafutio, usibaki kulalama,
Mungu akisema ndiyo, hakuna wa kuzuia.
Maisha ni harakati, riziki jitafutia,
Uchakarike ‘usweti’, mahali kupafikia,
Uchungu wa mkuyati, nao ukakuingia,
Mungu akisema ndiyo, hakuna wa kuzuia.
Katika mafanikio, hawakosi maadui,
Wale wafikiriao, kukutenda ubedui,
Wa mapembe masikio, nazo roho za utui,
Mungu akisema ndiyo, hakuna wa kuzuia.
Wa nukhsi nukhsani, mambo kukuharibia,
Wanoumia rohoni, mambo yakikunyokea,
Watemao mate chini, ukishaipita njia,
Mungu akisema ndiyo, hakuna wa kuzuia.
Wenye husuda rohoni, pindi ukifanikiwa,
Wenye kusema pembeni, ati umependelewa,
Daima wanotamani, wewe kuharibikiwa,
Mungu akisema ndiyo, hakuna wa kuzuia.
Wakeshao kwa waganga, kukufanyia mizungu,
Ili uweze boronga, maisha yawe machungu,
Wasochoka kusimanga, kukuwekea kiwingu,
Mungu akisema ndiyo, hakuna wa kuzuia.
Hakuna wa kuzuia, Mungu akishaamua,
Baraka kikujazia, wengine wajisumbua,
Watabaki kuumia, roho zikiwatufua,
Mungu akisema ndiyo, hakuna wa kuzuia.
Milango ‘kikufungia, siache kumwomba Mungu,
Yeye takufungulia, kokote chini ya mbingu,
Kheri atakujazia, hata iwe kwa mafungu,
Mungu akisema ndiyo, hakuna wa kuzuia.
Jifunze sana subira, ila sikose imani,
Omba sana kwa busara, umwombe yeye Manani,
Akwepushie madhara, na roho za wafitini,
Mungu akisema ndiyo, hakuna wa kuzuia.
Visa wakikufanyia, kamwe siwarudhishie,
Mola atakujalia, mabaya akwepushie,
Baya kikusingizia, Mola akusaidie,
Mungu akisema ndiyo, hakuna wa kuzuia.
Watahangaika bure, kama Mungu keshasema,
Vyao ni viherehere, na roho zikiwauma,
Waachie ziwafure, wewe zidi tenda mema,
Mungu akisema ndiyo, hakuna wa kuzuia.
Tayezuia ni nani, Mungu kishakuchagua,
Hawawezi abadani, wakeshe wakiagua,
Mungu siye Athumani, kila mtu amjua,
Mungu akisema ndiyo, hakuna wa kuzuia.
Usije kata tamaa, kisa wenye roho mbaya,
Waufanyao unaa, mambo kuharibikiya,
Wakwombeao balaa, waache waule chuya,
Mungu akisema ndiyo, hakuna wa kuzuia.
Hakuna wa kuzuia, Mungu akisema ndiyo,
Ukweli nimekwambia, kaziyo kujua hayo,
Yalo mema simamia, Mola ndiyo kimbiliyo,
Mungu akisema ndiyo, hakuna wa kuzuia.
No comments:
Post a Comment